1.Wakati nitakapo kumponya Israeli, ndipo yafunuliwapo maovu ya Efraimu, na ubaya wa Samaria; maana wanatenda uongo, na mwivi huvunja nyumba za watu, na kundi la wanyang'anyi hushambulia nje.
2.Wala hawafikiri mioyoni mwao ya kwamba naukumbuka uovu wao wote; sasa matendo yao wenyewe yamewazunguka pande zote; yako mbele za uso wangu.
3.Humfurahisha mfalme kwa uovu wao, na wakuu wao kwa uongo wao.
4.Hao wote ni wazinzi; wamekuwa kama tanuu iliyotiwa moto na mwokaji; huacha kuuchochea moto, tangu kuukanda unga hata umekwisha kutiwa chachu.
5.Sikukuu ya mfalme wetu, wakuu walijitapisha kwa ukali wa divai; alinyosha mkono wake pamoja na wenye mzaha.
6.Maana wamefanya moyo wao kuwa tayari kama tanuu, wakati waoteapo; hasira yao hulala usiku kucha; asubuhi yawaka kama moto utoao miali.
7.Wote wamepata moto kama tanuu, nao hula makadhi wao; wafalme wao wote wameanguka; hakuna hata mmoja wao aniitaye mimi.
8.Efraimu ajichanganya na mataifa; Efraimu ni mkate usiogeuzwa.
9.Wageni wamekula nguvu zake, naye hana habari; naam, nywele za mvi zimeonekana huko na huko juu yake, naye hana habari.
10.Na kiburi cha Israeli chamshuhudia mbele ya uso wake; ila hata hivyo hawakumrudia Bwana, Mungu wao, wala hawakumtafuta kwa ajili ya hayo yote.
11.Naye Efraimu amekuwa kama njiwa mpumbavu, asiye na fahamu; humwita Misri, huenda Ashuru.
12.Watakapokwenda nitatandika wavu wangu juu yao; nitawashusha kama ndege wa angani; nitawarudi, kama vile mkutano wao ulivyosikia.
13.Ole wao! Kwa kuwa wamenikimbia; uharibifu na uwapate! Kwa kuwa wameniasi; ingawa ninataka kuwakomboa, hata hivyo wamenena uongo juu yangu.
14.Wala hawakunililia kwa moyo, lakini wanalalamika vitandani mwao; hujikutanisha ili kupata nafaka na divai; huniasi mimi.
15.Ingawa nimewafundisha na kuwatia nguvu mikono yao, hata hivyo hukusudia udhalimu juu yangu.
16.Wao hurudi, lakini si kwake Aliye juu; wamekuwa kama upinde usiotumainika; wakuu wao wataanguka kwa upanga, kwa sababu ya jeuri ya ndimi zao; jambo hili litakuwa kwao sababu ya kuchekwa katika nchi ya Misri.